Tuesday, January 10, 2012

TFF MNYIKA AIPA  CHNGAMOTO TFF

na Mwandishi wetu
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetakiwa kuweka mkazo kwa klabu za ligi kuu na daraja la kwanza ziweze kushuka hadi ngazi ya mitaa kwa ajili ya kusaka vipaji vya soka badala ya kukimbilia nyota wa nje ya nchi.

Wito huo umetolewa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika jana, wakati akikabidhi zawadi kwa washindi wa mashindano ya Ntinika Cup, timu ya Black Lion ya Mbezi Makabe baada ya kuilaza Home Boys ya Mtaa wa Msumi mabao 2-1 katika fainali ya michuano hiyo kwenye viwanja vya Mbezi.

Mnyika alisema, endapo mamlaka husika zingekuwa zinasaka vipaji vya wachezaji toka ngazi ya chini, badala ya kukimbilia majina makubwa ambayo yamekuwa na desturi ya kuwaangusha kila mara, soka la Tanzania lingeweza kupiga hatua zaidi, kwani mitaani kuna vipaji vingi vinavyokosa njia ya kujiendeleza.

“Mbona miaka ya sabini hatukuwa na wachezaji wa nje na vilabu vilikuwa vinafanya vizuri, sasa ni kitu gani kinashindikana au ni kukosa uzalendo kwa wachezaji wetu wa sasa na katika hili, inatupasa tuiambie TFF warudishe misingi ya kusaka vipaji ngazi za chini,” alisema Mnyika.

Aidha, mbunge huyo alitoa wito kwa Manispaa ya Kinondoni, kuboresha viwanja vya michezo, kuwawezesha vijana kutoka wilaya hiyo kucheza kwenye viwanja vyenye ubora.

Kwa upande wake, Mratibu wa mashindano hayo, Nicholaus Ntinika, alisema, lengo la mashindano hayo lilikuwa kukuza vipaji vya vijana wa Kata ya Mbezi, ikiwa ni pamoja na kuwafanya watambuane kwa ajili ya kusaidiana katika masuala mbalimbali ya kijamii.

Timu 20 za mitaa mbalimbali ya Kata ya Mbezi zilishiriki michuano hiyo, ambako mshindi wa kwanza alijipatia Kombe, jezi seti moja, mpira moja na fedha taslimu sh 100,000.